Leo tutazame katika swala la dhana ya Elimu na maana yake kwa ujumla,je wewe unadhani Elimu ni nini?
Wataalamu na wadau mbalimbali wa Elimu, wametafsiri dhana ya Elimu katika maana tofauti tofauti.kuna waliosema Elimu ni:
*Tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi.
*Ni mchakato mzima unaowezesha kujifunza
*Utajiri wa maarifa anaoupata mtu binafsi baada ya kujifunza mambo fulani,masomo au kupitia michakato ya maisha katika mazingira yake.
*Tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi.
*Ni mchakato mzima unaowezesha kujifunza
*Utajiri wa maarifa anaoupata mtu binafsi baada ya kujifunza mambo fulani,masomo au kupitia michakato ya maisha katika mazingira yake.
Wengine wamedadavua kwa undani zaidi kuwa Elimu ni ukuzaji wa ufahamu
wa binadamu (enlightment).Ukuzajiwa ufahamu huu ambao unapaswa
kumpelekea binadamu na kumfanya binadamu kutenda katika usahihi , ili
kumfanya binadamu awe binadamu bora zaidi na mwenye kuzalisha na mwenye
faida kwake binafsi kwa taifa lake na kwa familia yake.
Yote haya ni majibu yaliyo sahihi lakini jibu sahihi zaidi kuhusu
dhana hii ya Elimu ni jumla ya maarifa,stadi na mielekeo inayotawaliwa
na mila na desturi za jamii ambapo binadamu huweza kupata kwa kujifunza
mwenyewe, kufundishwa na kwa njia nyingine.
Mtu mwenye Elimu huwa na taaluma au mbinu ambazo mtu huyo hufuata na kutumia katika kutatua matatizo yanayomzunguka.
Mfumo wetu wa kielimu wengi unatutengeneza kufikiri elimu ni
maarifa ya kazi peke yake ambayo yatatupatia kipato. Huku tukisahau
kabisa kwamba elimu ni zaidi ya hapo tunapodhania. Tukiishia katika
fikra za kwenda shule kusudi tupate kazi na kupata pesa kwa ajili ya
matumizi yetu ya kila siku tu, ndipo linapokuja suala la bora Elimu na
si Elimu bora.
Elimu bora hukuza ufahamu wa mwanadamu.Ukuaji huu wa ufahamu
hupelekea mabadiliko chanya ya mwanadamu huyu kifikra,maono na mitazamo
katika jamii inayomzunguka hivyo kumfanya binadamu huyu kutenda katika
usahihi kulingana na maadili ya jamii hiyo, na kumfanya mwanadamu huyu
kuwa bora zaidi na mwenye kuzalisha kwa faida ya kwake binafsi kwa
familia,jamii yake na taifa kwa ujumla.
Elimu bora atakayopata mwanadamu huyu kwanza itamwezesha kuitazama na
kuiongoza familia yake vizuri. itamwezesha kuwa na mahusiano mazuri na
jamii inayomzunguka pia na taifa kwa ujumla hivyo kumwezesha kuwa mtu
bora na mzalishaji kwa taifa. Ndio msingi wa elimu.
Mwanadamu huyu mwenye Elimu bora tunamtegemea,awe na uwezo wa
kuchanganua kati ya mambo yaliyo sahihi na yale yaliyo mapotofu, na
ataamua bila kusita kufuata mambo ambayo ni sahihi na kuacha kabisa
mambo yaliyo potofu.
Mwanadamu huyu tunategemea atakuwa na uwezo pia wa kutatua matatizo
yake yeye mwenyewe,matatizo yanayoikumba familia yake na jamii yake kwa
ujumla, mwanadamu huyu ni mtu ambaye mwenye elimu bora.Mwenye uwezo wa
kufahamu na kuchanganua mambo na kutenda katika usahihi.
Mwenye uwezo wa kuitazama familia yake vizuri, mwenye uwezo wa kuwa
na mahusiano mazuri na jamii inayomzunguka, mwenye uwezo wa kuwa raia
bora na mtu bora ambaye anazalisha katika taifa lake.
Tunapowapa watu elimu yatupasa kuangalia tabia za watu wetu na
kuzijenga katika usahihi. ni muhimu elimu yetu pamoja na kuangalia stadi
za ufanyaji wa kazi kwao lakini zijenge tabia zao. Hii italeta manufaa
kwa taifa na sio hasara. Kama tunawapa stadi za ufanyaji kazi tu watu
wetu lakini wanakuwa hawana manufaa kwa taifa letu bali ubinafsi na
hasara basi hiyo elimu ina kasoro tuitazame upya.
Elimu bora itamfanya mtu kutenda katika usahihi.Elimu
ambayo sisi kama taifa tunapaswa kuijenga. Na watoto wetu watakuwa
wenye akili kama wakipata elimu kama hiyo. Ni elimu ambayo itawalinda
dhidi ya maangamizi, itawalinda dhidi ya uovu.Lakini pia itawapa ujuzi
wa kufanya kazi.
Kwahiyo tukizalisha watu wenye Elimu bora,tutegemee viongozi wazuri,
watu wenye ujuzi wa hali ya juu kazini waaminifu na wenye maadili na
nidhamu ya kutosha.
Vinginevyo elimu ambayo itampa tu mtu ujuzi wa kazi pasipo mambo mengine ni sawasawa na kutwanga maji kwenye kinu.Elimu bila maadili ni sawasawa na mtu bila kiungo.Haitokuwa na faida. Itapotea tu.
Kuelimika ni kuondokana na matendo ya kijinga yasiyo na faida. Dhana
ya elimu ni kuondokana na ujinga. Na tunapima faida ya kitu kutokana na
matokeo ya kila matendo tunayofanya. Ili twende mbele kama taifa lazima
tuelimike. Tuachane na ujinga na tutende katika usahihi.
Hivyo ni Muhimu sana tunapotoa elimu, kuangalia tabia na dihamu za
watu wetu ili kuzijenga katika kutenda kiusahihi. Nidhamu,maadili na
uzalendo huleta mwelekeo iwe kwa taifa au kwa mtu binafsi.
No comments:
Post a Comment